ABOUT THE AWARDS
Picture Gallery Send us feedback
Historia fupi ya Tuzo za Muziki Tanzania Soma kwa kiingereza

TUZO za muziki nchini maarufu kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards (TMA) zilianzishwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mwaka 1999 kama kichocheo cha kutambua wanamuziki nchini na kazi zao.

Wajibu wa serikali katika tuzo za muziki - Tanzania Music Awards:

Serikali kwa kupitia wizara ya Elimu na utamaduni na asasi yake ya BASATA ina mamlaka na wajibu wa kufufua,kuhifadhi, kuendeleza maadili ya kisanii yaani kuendeleza utamaduni.

Kutokana na hilo tuzo za muziki Tanzania, zinakuwa ni sehemu ya wajibu wake kwa jamii katika kuendeleza na kuhifadhi muziki wa Kitanzania (yaani kwa kuanzisha michuano ya kimkoa au kikanda katika tuzo nzima za muziki) na hivyo kuhifadhi maadili kwa kupitia muziki.

Serikali kwa kupitia wizara yake husika na asasi yake ya BASATA ina wajibu wa kutoa ruhusa,"Vibali" kwa waandalizi wa tukio zima la tuzo za muziki kama sehemu ya uendelezaji wa shughuli za kisanii nchini.

Serikali pia kwa kupitia wizara yake na asasi husika, BASATA ina wajibu wa kuratibu matukio yote yanayohusu tuzo hizi za muziki kuanzia ngazi ya kikanda hadi kitaifa.

Pia serikali ina wajibu wa kusaidia waandalizi wa tukio, Kamati ya TMA na washiriki wengineo katika tuzo hii,katika masuala ya kiufundi ili kufanikisha utoaji wa tuzo kwa kuwa yenyewe ina wataalamu waliobobea katika fani husika kwa kuzingatia sera ya utamaduni iliyopo.

Sera ya utamaduni, Kifungu cha 4, kifungu kidogo 4.1.4 serikali kwa kushirikiana na TMA inatekeleza wajibu wake kwa kuanzisha mfumo unaotambua na kuenzi wasanii wa kitaifa.

BASATA ni chombo kilichopo chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni kikiwa na kazi kubwa ya kukuza na kuhifadhi sanaa na utamaduni wa Mtanzania.

Baada ya kuanzisha tuzo hizo mwaka 1999, BASATA kwa kushirikiana na "Serengeti Promotions" chini ya uongozi wake Bw. John Kagaruki walianza harakati za kufanikisha utoaji wa tuzo.

Tuzo mbalimbali zilitolewa kwa kuzingatia kazi ya msanii husika zilizofanywa kati ya Januari na Desemba 1998. Tukio la utoaji tuzo lilihitimisha kalenda ya muziki kwa ngazi ya kitaifa.

Mfumo ule ule wa kutoa tuzo kwa wasanii kwa kuzingatia kazi za mwaka uliopita, ndio ambao uliendelea kutumika katika matukio ya kila mwaka ya utoaji wa Tuzo za Muziki (TMA) nchini.

Mwaka 2000 Look Promotion chini ya uongozi wa Mbamba Uswege wakishirikiana na Clouds FM walipata nafasi ya kuandaa tuzo hizo.

Katika mwaka wake wa tatu wa utoaji wa tuzo hiyo yaani mwaka 2002, kampuni ya uendelezaji sanaa ya Dandu Planet Africa, chini ya uongozi wake marehemu James Dandu iliomba kuandaa tukio hilo kwa kushirikiana na Robert Zangi ambaye baadaye alikuja kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi.

Tukio la utoaji tuzo liliandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na kampuni ya bia nchini, TBL, kwa kupitia udhamini wa bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager.

Tukio hilo lilifanyika kwa ufanisi na kuleta mafanikio makubwa kwa wanamuziki na wapenzi wa muziki nchini.

Dandu Planet Africa iliomba tena kuandaa tukio la mwaka 2002 ambalo lilikusudiwa kufanywa Machi 28, 2003.

Tukio la mwaka 2003 la utoaji tuzo za Tanzania Music Awards chini ya udhamini wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager lilikuwa tena na mafanikio makubwa. Hii ni pamoja na kutanua wigo wa muziki na washiriki wake.

Kwanza, idadi ya nafasi zinazogombewa katika tuzo hizo ziliongezwa kufikia 31 na pili tuzo zililenga kuwatia hamasa pia wanamuziki wanaochipukia mikoani na pia kuwa na ongezeko la ushindani kikanda.Maafisa wa BASATA na maafisa utamaduni wa wilaya kutoka Mwanza , Mbeya na Arusha walishiriki.

Kulikuwa na mafanikio zaidi mwaka 2003, lakini kubwa zaidi ni lile la tuzo kuambatana na kiwango kikubwa cha fedha taslimu.

Tanzania Music Awards iliboreshwa zaidi na kuwa na zawadi ya fedha taslimu ya zaidi ya shilingi za Kitanzania 10,500,000/=.

BASATA kwa hali hiyo, ilifanikisha kupeleka ushawishi kwa wasanii kwa namna ya pekee kutengeneza kazi bora kabisa ambazo zitapata nafasi si katika mioyo yao tu bali pia kitaifa na nje ya nchi.

Mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu tuzo hizo kuingia katika udhamini wa TBL kwa kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager ifuatavyo.

  • Thamani ya tuzo na vinavyoambatana navyo kifedha zimepanda na kufikia zaidi ya Tsh. 10,500,000/=
  • Tuzo zimefikishwa ngazi za kimkoa ili kuweza kuwaendeleza wanamuziki chipukizi na wale ambao hawajajulikana nchini kote.
  • Kuanzishwa kwa Kamati yenye uwezo wa kufanikisha maadhimisho ya tuzo kila mwaka.
  • Kuendeleza zaidi nafasi mbalimbali za tuzo kwenda sambamba na zile za kimataifa zinazotambulika
  • Kuanzisha eneo la wasanii maarufu kwa ajili ya wanamuziki ambao wamechangia ukuzaji na mafanikio ya muziki wa Tanzania.

 

 
Designed and powered by INFOCOM TECHNOLOGIES LTD.