Picture Gallery Send us feedback

NEWS

Ali Kiba, Lady Jay Dee watamba tuzo za Kili

Wasanii Ali Kiba na Judith Wambura ambao kwa sasa wapo barani Ulaya kwa shughuli za kikazi, juzi usiku walitwaa tuzo za Kili Music jijini, Dar es Salaam.

Wimbo wa Cinderella ulimpatia tuzo chipukizi huyo baada ya kushinda katika kipengele cha Wimbo bora wa R\'n\'B, ambacho licha ya wimbo huo, zingine zilizokuwa zikigombea ni Bembeleza wa Marlaw, Binti Kiziwi wa Z Anto, Haiwezekani ya Kassim pamoja na Wachuja ulioimbwa kwa ushirikiano kati ya Queen Darleen na Ali Kiba.

Judith Wambura alishinda tuzo ya mwimbaji bora wa kike, akiwapiga kumbo Irene Sanga, K Lynn, Luiza Mbutu na Sikudhan Ally.

Wakati Kiba kwa sasa yupo Ujerumani, Lady Jay Dee alikuwa London alikoshiriki tamasha la kumbukumbu ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela anayefikisha umri wa miaka 90.

Wengine waliopata tuzo jana na vipengele vyao ni Jahazi Modern Taarabu iliyoibuka kidedea katika albamu bora ya taarabu, Marlaw (mwimbaji bora wa kiume), Dar ModernTaarabu iliyoibuka bingwa kwenye wimbo bora wa taarab kwa wimbo wake wa Gharika ya moyo.

Marlaw pia aliibuka kidedea katika wimbo bora wa mwaka baada ya kushinda kwa wimbo wake wa Bembeleza, Khalid Chokoraa alichanua katika wimbo bora wa kiswahili bendikwa kibao chake cha Kuachwa huku African Stars ikitwaa tuzo kwa albamu bora ya Mtaa wa kwanza.

Wimbo bora wa asili wa Kitanzania ulikwenda kwa Kalunde Band iliyoshinda na kibao chake cha Itumba Mbwene, Albamu bora ya asili ilichukuliwa na Maringo Band kwa albamu yao ya Kisiwa cha Ukerewe na msanii Fid Q aliibuka kinara katika mchuano wa wimbo bora wa Hip hop kwa kibao chake cha Ni hayo tu

.

 
Habari zaidi